Deuteronomy 14

Vyakula Vilivyo Najisi Na Vilivyo Safi

(Walawi 11:1-47)

1 aNinyi ni watoto wa Bwana Mwenyezi Mungu wenu. Msijichanje ama kujinyoa upara kwenye paji la uso kwa ajili ya aliyekufa, 2 b ckwa maana ninyi ni taifa takatifu kwa Bwana Mwenyezi Mungu wenu. Bwana amewachagua ninyi kuwa taifa la kipekee kutoka mataifa yote juu ya uso wa dunia, mwe tunu yake.

3 dMsile kitu chochote ambacho ni machukizo. 4 eHawa ndio wanyama mtakaokula: ng’ombe, kondoo, mbuzi, 5 fkulungu, paa, kongoni, paa mweupe, mbuzi-mwitu, pofu na kondoo wa mlimani. 6Mnaweza kumla mnyama yeyote mwenye kwato zilizogawanyika mara mbili, pia yule anayecheua. 7Hata hivyo, miongoni mwa wale wanaocheua au wale walio na kwato zilizogawanyika kamwe msile ngamia, sungura na pelele. Iwapo wanacheua, lakini hawana kwato zilizogawanyika; ni najisi kwenu kwa taratibu za kiibada. 8 gNguruwe pia ni najisi; ingawa ana kwato zilizogawanyika, hacheui. Msile nyama yake wala kugusa mzoga wake.

9Katika viumbe hai vyote viishivyo kwenye maji, mnaweza kula yeyote aliye na mapezi na magamba. 10Lakini chochote kisicho na mapezi na magamba msile; kwenu ni najisi.

11Mnaweza kula ndege yeyote aliye safi. 12 hLakini wafuatao msiwale: tai, furukombe, kipungu, 13 ikengewa mwekundu, kengewa mweusi, mwewe wa aina yoyote, 14 jkunguru wa aina yoyote, 15mbuni, kiruka-njia, dudumizi, kipanga wa aina yoyote, 16bundi, mumbi, bundi mkubwa, 17 kmwari, nderi, mnandi, 18korongo, koikoi wa aina yoyote, hudihudi na popo.

19Wadudu wote warukao kwa makundi ni najisi kwenu, msiwale. 20 lLakini viumbe vyote vyenye mabawa vilivyo safi mwaweza kula.

21 mMsile kitu chochote mtakachokuta kimekufa. Mnaweza kumpa mgeni yeyote anayeishi katika mojawapo ya miji yenu, naye anaweza kula au mnaweza kumuuzia mtu wa nchi nyingine. Lakini ninyi ni watu watakatifu kwa Bwana Mwenyezi Mungu wenu.

Msitokose mwana-mbuzi katika maziwa ya mama yake.

Zaka

22 nHakikisheni mmetenga sehemu ya kumi ya mazao yote ya mashamba yenu kila mwaka. 23 oMtakula zaka za nafaka yenu, divai mpya, mafuta na wazaliwa wa kwanza wa makundi yenu ya ng’ombe na ya kondoo na mbuzi mbele za Bwana Mwenyezi Mungu wenu pale mahali atakapopachagua kama maskani kwa ajili ya Jina lake, ili kwamba mpate kujifunza kumheshimu Bwana Mwenyezi Mungu wenu daima. 24 pLakini ikiwa mahali pale ni mbali sana nanyi mmebarikiwa na Bwana Mwenyezi Mungu wenu na hamwezi kubeba zaka yenu (kwa sababu mahali pale Bwana atakapopachagua kuliweka Jina lake ni mbali sana), 25 qbasi badilisheni zaka yenu kuwa fedha, mkaichukue hiyo fedha mwende nayo mahali Bwana Mwenyezi Mungu wenu atakapopachagua. 26 rTumieni hiyo fedha kununua chochote ukitakacho: ng’ombe, kondoo, divai au kinywaji chochote chenye chachu au chochote mnachotaka. Kisha ninyi na wa nyumbani mwenu mtaila mbele za Bwana Mwenyezi Mungu wenu na kufurahi. 27 sMsiache kuwajali Walawi waishio katika miji yenu, kwa kuwa hao hawana shamba wala urithi wao wenyewe.

28 tMwishoni mwa kila mwaka wa tatu, leteni zaka zote za mazao ya miaka ile na uyahifadhi kwenye miji yenu, 29 uili Walawi (ambao hawana mashamba wala urithi wao wenyewe) na wageni, yatima na wajane wanaoishi kwenye miji yenu wapate kuja kula na kushiba, ili Bwana Mwenyezi Mungu wenu apate kuwabariki ninyi katika kazi zote za mikono yenu.
Copyright information for SwhKC